MBUNGE
wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) jana alijisalimisha Kituo
Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam kwa ajili ya kuhojiwa kutokana na kauli
za uchochezi alizozitoa, lakini akakosa dhamana.
Hatua
ya Lissu kukosa dhamana na kulala rumande imekuja siku moja baada ya
kuachiwa kwa dhamana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
anakokabiliwa na mashitaka ya kuchapisha taarifa za uchochezi katika
gazeti la Mawio.
Alifika
kituoni hapo jana saa 7.38 mchana akiwa katika gari aina ya BMW lenye
namba za usajili T549 BHH na kuhojiwa kwa saa tatu mfululizo juu ya
kauli yake ya kumuita Rais John Magufuli kuwa ni dikteta ‘uchwara’,
kuandika uchochezi katika mitandao ya kijamii na kutoa kauli za kuudhi.
Kwa
mujibu wa Mwanasheria wa Lissu, John Mallya, kilichomfanya Lissu alale
rumande ni kutokana na polisi kudai kuwa amefanya uchochezi na kutumia
lugha ya kuudhi ya kusema kuna mtu anaitwa dikteta uchwara.
“Lissu
amezungumza msingi wa kwa nini amesema dikteta uchwara kwenye mahojiano
yake na amerekodiwa katika nyaraka za kipolisi na amehojiwa kwa saa
tatu kuhusu jambo hilo, na kauli aliyosema jana kutoka mahakamani,”
alisema Mallya.
Alisema
wao kama wanasheria wataendelea kumpigania Lissu na kama atafikikishwa
mahakamani leo watakuwepo kuhakikisha anapata haki zake zote za
kisheria. Mallya alidai hakuna ujumbe wowote alioandika Lissu uliokuwa
unasababisha uchochezi.
Awali,
Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema ambaye alikuwepo kituoni hapo,
alidai hakuna jambo baya ambalo wanaona Lissu kalizungumza, bali
alichokifanya ni kusema mtazamo wake kwa jinsi anavyoona.
Alisema
chama hicho kitaendelea kuikosoa serikali pale kitakapoona mambo
hayaendi sawa ili kuhakikisha serikali inasimama katika hali ambayo kila
mmoja ataridhishwa nayo.
Juzi
katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Lissu aliachiwa kwa dhamana
katika kesi ya inayomkabili ya mashitaka ya kuchapisha taarifa za
uchochezi katika gazeti la Mawio, akijumuishwa kwenye kesi hiyo akiwa na
washtakiwa wenzake ambao ni mwandishi wa habari hizo, Jabir Idrissa,
Mhariri wa gazeti hilo, Simon Mkina na Mchapishaji wa Kampuni ya Jamana,
Ismail Mehboob.
0 comments:
Post a Comment