Thursday, 30 June 2016

MBUNGE wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) jana alijisalimisha Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam kwa ajili ya kuhojiwa kutokana na kauli za uchochezi alizozitoa, lakini akakosa dhamana.

Hatua ya Lissu kukosa dhamana na kulala rumande imekuja siku moja baada ya kuachiwa kwa dhamana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu anakokabiliwa na mashitaka ya kuchapisha taarifa za uchochezi katika gazeti la Mawio.

Alifika kituoni hapo jana saa 7.38 mchana akiwa katika gari aina ya BMW lenye namba za usajili T549 BHH na kuhojiwa kwa saa tatu mfululizo juu ya kauli yake ya kumuita Rais John Magufuli kuwa ni dikteta ‘uchwara’, kuandika uchochezi katika mitandao ya kijamii na kutoa kauli za kuudhi.

Kwa mujibu wa Mwanasheria wa Lissu, John Mallya, kilichomfanya Lissu alale rumande ni kutokana na polisi kudai kuwa amefanya uchochezi na kutumia lugha ya kuudhi ya kusema kuna mtu anaitwa dikteta uchwara.

“Lissu amezungumza msingi wa kwa nini amesema dikteta uchwara kwenye mahojiano yake na amerekodiwa katika nyaraka za kipolisi na amehojiwa kwa saa tatu kuhusu jambo hilo, na kauli aliyosema jana kutoka mahakamani,” alisema Mallya.

Alisema wao kama wanasheria wataendelea kumpigania Lissu na kama atafikikishwa mahakamani leo watakuwepo kuhakikisha anapata haki zake zote za kisheria. Mallya alidai hakuna ujumbe wowote alioandika Lissu uliokuwa unasababisha uchochezi.

Awali, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema ambaye alikuwepo kituoni hapo, alidai hakuna jambo baya ambalo wanaona Lissu kalizungumza, bali alichokifanya ni kusema mtazamo wake kwa jinsi anavyoona.

Alisema chama hicho kitaendelea kuikosoa serikali pale kitakapoona mambo hayaendi sawa ili kuhakikisha serikali inasimama katika hali ambayo kila mmoja ataridhishwa nayo.

Juzi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Lissu aliachiwa kwa dhamana katika kesi ya inayomkabili ya mashitaka ya kuchapisha taarifa za uchochezi katika gazeti la Mawio, akijumuishwa kwenye kesi hiyo akiwa na washtakiwa wenzake ambao ni mwandishi wa habari hizo, Jabir Idrissa, Mhariri wa gazeti hilo, Simon Mkina na Mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehboob.

Advertisement
==

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Mpekuzi Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana

RAIS Dk. John Magufuli amemtumbua mfanyabiashara mmoja maarufu Dar es Salaam, aliyebainika kufanya miamala ya fedha ya Sh milioni saba hadi nane kwa kila baada ya dakika moja.

Kutokana na hesabu ya Sh milioni saba anayoingiza kwa dakika moja, mfanyabiashara huyo hutengeneza Sh milioni 420 kwa kila saa moja, sawa na Sh bilioni 5.2 kwa saa 12 na Sh trilioni 16 kwa mwezi ambazo halipi Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).

Rais Magufuli amesema mfanyabiashara huyo aliyebainika kuwa na makampuni mengi, alikuwa akishirikiana na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni nchini (BRELA) pamoja na Mamlaka ya ato Tanzania (TRA).

Mkuu huyo wa nchi alitoa kauli hiyo Ikulu, Dar es Salaam jana, baada ya kuwaapisha wakuu wapya wa mikoa watatu katika hafla iliyohudhuriwa pia na wakuu wa wilaya wateule.

Alisema waligundua jipu hilo baada ya kufuatilia kwenye mapato.

“Tulikuwa tunafuatilia kwenye ‘revenue’ (mapato), kwenye zile VAT ambazo zinatumika ‘ku-collect revenue’ (kukusanya mapato), yupo mtu mmoja ambaye alikuwa ametengeneza kampuni zake nyingi, alikuwa anafanya ‘transaction’ (miamala) ya fedha kila dakika moja kati ya Sh milioni saba na nane.

“Na hizo risiti alikuwa anaziuza kwa wafanyabiashara wengine, kwenye VAT anatakiwa kulipia kwa asilimia 18. Wafanyabiashara wengine hao walikuwa wanauziwa kwa asilimia tano na wakishauza bidhaa wanakwenda kuomba TRA iwarudishie hiyo asilimia 18, kwa hiyo Serikali imekuwa ikipoteza asilimia 18.5, ni matrilioni na matrilioni ‘of money’ (ya fedha).

“Bahati nzuri huyo mtu yuko kwenye mikono salama, tunafuatilia namna tutakavyorudisha hizo fedha, na huyo mtu alikuwa ana-connection kati ya watu wa BRELA na TRA… hiyo ndiyo Tanzania.

“Najaribu tu kutoa mfano ili katika maeneo yenu mkasimamie mapato ya Serikali, kwa sababu tumepoteza mapato mengi kuliko tunavyofikiria, huku Watanzania wakiteseka sana, na mambo yanayofanyika ni ya ajabu,” alisema Rais Magufuli akiwaambia wakuu hao wa mikoa na wilaya.

Pamoja na mambo mengine, Rais Magufuli alisema mchakato wa kupata wakuu wapya wa wilaya ulikuwa mgumu, na kwamba amewaacha wengi wa zamani kwa kuwa hawakutimiza vigezo alivyovitaka.

“Mchakato wa kupata ma-DC ulikuwa mgumu kwa sababu ilibidi tuangalie historia ya kila mmoja. Tuliangalia mambo mengi sana, lakini pia tuliangalia kwa ku-preview atatimiza haya tunayotaka kuyafanya kwa miaka mitano?

“Na ndiyo maana mnavyoona ma-DC wa zamani waliorudi ni 39, kwa hiyo wale 101 wote hawakurudi… niseme tu ukweli kwamba hawakufikia vigezo tulivyokuwa tunavitaka,” alisema Rais Magufuli.

Alisema katika uteuzi huo, alichukua wakurugenzi kwa kuwa walifanya vizuri katika maeneo yao waliyokuwa wakiyaongoza.

“Tulichukua wakurugenzi walio-perform vizuri katika maeneo yao. Wapya wako takribani 100 na waliobaki ni hao kati ya 38 na 39. Ni matumaini yangu kwamba mtakwenda kufanya kazi na kutimiza wajibu wenu.

“DC ni nafasi kubwa ya uongozi katika Serikali na ndiyo maana mfano mkubwa wa DC mstaafu ni Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa), ni kwa sababu alitimiza wajibu wake na leo yuko hapa,” alisema.

Mkuu huyo wa nchi aliwapa mikakati ya kufanya kazi wakuu hao wa wilaya kwa kutimiza dhana ya kuchapa kazi kwa niaba ya Serikali.

“Nina matumaini makubwa mtakwenda kutimiza dhana ya kuchapa kazi kwa niaba ya Serikali, ninyi ndio wawakilishi wetu na ndio mnawakilisha wananchi wa maisha yote.

“Watanzania wana matatizo na changamoto kubwa. Ni matumaini yangu kwamba hamtaniangusha na hamtaiangusha Serikali. Nina imani mtakwenda kutatua matatizo ya wananchi, hasa walio masikini, sitegemei wala sifikirii kwamba mkawe chanzo cha kutengeneza matatizo,” alisema Rais Magufuli.

Kutokana na hali hiyo, aliwataka wasimamie haki, huku wakimtanguliza Mungu katika kufanya kazi, kusimamia maadili, kutenda haki, kutojihusisha na rushwa, kuwatumikia Watanzania bila kubagua dini, kabila wala vyama vyao.

“Kikubwa mkasimamie yale tuliyoyaahidi sisi wanaCCM, kwa sababu wakati tunazunguka tukiomba kura, yapo tuliyoyaahidi, hayo mkayatekeleze kwa nguvu zote.

“Na wala asitokee mtu yeyote wa kuwakwamisha kutekeleza hayo, ninyi ndio wakuu wa wilaya na ninyi watatu ndio wakuu wa mikoa. Mna mamlaka makubwa ya kuweka mahabusu mtu masaa 48 halafu kesho yake ukamwachia. Ila msiende kuonea watu, mkachape kazi.

“Imani tuliyoionyesha kwenu sisi viongozi wenu mkaionyeshe kwa Watanzania mnaowaongoza, mkashirikiane na viongozi mtakaowaongoza, wanasema umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu.

“Nina uhakika mkisimama vizuri  kwa kuzingatia maadili mliyonayo, na bahati nzuri wengi mna uzoefu katika maeneo yenu. Mkawahamasishe Watanzania katika wilaya na mikoa yenu kufanya kazi. Watanzania wengi tumezoea kulalamika, tunataka tupewe, lakini hatufanyi kazi. Tukawasimamie kuchapa kazi,” alisema.

Aliwataka wakuu hao wa wilaya ambao pia ni wenyeviti wa kamati ya ulinzi na usalama, kukemea rushwa katika maeneo yao na kusimamia mapato ya Serikali.

“Huwa inatokea saa nyingine wakurugenzi kwa sababu kuna fedha nyingi tunapelekaga kule, wanadhani ni zao wakati ni za Serikali, mkawasimamie bila woga.

“Kupitia halmashauri zenu, mkahakikishe fedha hizo zinatumika kulingana na matakwa ya kanuni na sheria za nchi,” alisema Rais Magufuli.


Advertisement
==

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Mpekuzi Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Wabunge wa Kambi Rasmi ya Upinzani leo asubuhi wameingia bungeni wakiwa wote wamevalia nguo nyeusi walipohudhuria kikao cha 54 cha Bunge la Bajeti mjini Dodoma.

Baada ya Naibu Spika Dk Tulia Ackson kuingia bungeni na kuongoza dua ya kuliombea Bunge, walianza kunyanyua mabango mbalimbali na kutoka nje.

Saturday, 18 June 2016


Uzimaji wa Imei bandia ulifanyika usiku wa kuamkia jana kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) katika simu zaidi ya 600,000 zenye Imei batili. 
Kwa mujibu wa TCRA, Imei ni namba ya kimataifa ya utambuzi wa vifaa vya kielektroniki, ikiwamo simu. Ina tarakimu 15 ambazo ni za kipekee kwa kifaa husika na zinatambulika kimataifa. Namba hizo hutumika kudhibiti bidhaa bandia au simu kutumiwa na mtu mwingine. 
Jana, Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano wa TCRA, Innocent Mungy alisema takwimu hizo ni zile ambazo zimetokana na kazi ya kukata mawasiliano katika simu bandia iliyofanyika kuanzia saa sita usiku mpaka saa kumi alfajiri ya jana. 
Alisisitiza kuwa mtambo huo unaendelea na kazi kuhakikisha kuwa hata simu ambazo hazipo au hazikuwa hewani zitakapowashwa hazitafanya kazi. 
“Kazi ya kuzima simu hizo ilianza usiku wa kumkia jana saa sita usiku na kila kampuni ya mtandao wa simu ilipaswa kuzima simu za wateja wake ambazo ni feki na kazi ya mtambo ni kuhakikisha simu iliyozimwa inapowekewa kadi ya mtandao mwingine haifanyi kazi na kuhakikisha simu zote feki zitakazoingia nchini hazifanyi kazi,” alisema Mungy. 
Hata hivyo, kuna baadhi ya wamiliki wa simu ambao walitilia shaka ufanisi wa mtambo huo kwa madai kuwa tayari walishathibitishiwa na TCRA kwamba simu zao ni feki, lakini bado zinafanya kazi. 
“Simu yangu mimi niliangalia nikaambiwa ni feki na niibadilishe kabla ya tarehe 16 Juni, lakini jana wamezizima feki ya kwangu bado inafanya kazi kama kawaida napiga na kupokea simu kama zamani,” alisema Nael Joseph. 

Kuhusu suala hilo, Mungy alisema: “Hoja hizo zimejitokeza kwa wingi na wengine walifikia hatua ya kuushutumu mtambo wetu kuwa ni feki na kuwa umeshindwa kuzima simu feki ukazima orijino, lakini ukweli ni kwamba mtambo ule hauzimi kama taa au kama ule uliozima matumizi ya analojia bali unazima taratibu

"Niweke sawa kwamba mtambo huu hauonei mtu na unazima simu zote zilizo feki.” 

Mungy aliongeza kuwa wengi wamekuwa hawaelewi mantiki ya ujumbe wa uthibitisho.Alisema ujumbe unamtaka mmliki wa simu kuoanisha jina linalotajwa kama ndilo jina halisi la simu yake. “Kama jina linalotajwa na Imei linaoana na lililoandikwa kwenye simu yako, basi sio feki, lakini majina yakiwa hayafanani ndipo simu inakuwa feki,” alifafanua. 
Vodacom wazungumza 
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Vodacom, Rosalynn Mworia alisema walipewa jukumu la kuzima simu feki za wateja wao na TCRA.
“Jana saa sita usiku tulitekeleza agizo kama lilivyotolewa na TCRA na inavyoonekana wengi wao walikuwa wamejipanga kwani simu nyingi zimezimwa, lakini baadhi wamerejea hewani japokuwa wapo ambao mpaka sasa hawajarudi,” alisema Mworia .
Seebait.com 2016SeeBait

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema waendesha bodaboda na abiria wasiovaa helmet watakamatwa na kushtakiwa kwa kosa la kutaka kujiua.
Makonda aliyemwakilisha Makamu wa Rais kwenye futari iliyoandaliwa na Benki ya NMB kwa wateja na wadau wake juzi, alisema abiria na wapanda vyombo hivyo wanatakiwa kuvaa helmet.

Alisema kupanda pikipiki bila usalama ni kwamba abiria anadhamiria kujiua, kwa sababu akipata ajali ni rahisi kupoteza maisha kwa kupiga kichwa chini.

“Nimeshawasiliana na kamati yangu ya usalama barabarani mkoa, hili nitalisimamia kikamilifu lazima wote wawe na helmet na wakikamatwa wote watashtakiwa,” alisema.

Mkuu huyo wa mkoa alisema kupanda bodaboda bila kuvaa kofia hiyo, ni sawa na mtu anayechukua vidonge na kunywa na pombe kali, ambayo matokeo yake ni kifo.

Makonda alisema kazi hiyo ataifanya kipindi hiki cha Mfungo wa Ramadhani ili apate thawabu ikiwamo kuruhusu maduka makubwa kufanya kazi hadi usiku wa manane.

Alisema hiyo itasaidia wanaofanya kazi wakirudi nyumbani wanafuturu baadaye wanaswali Tarawehe, hivyo wanaweza kwenda kufanya manunuzi usiku.

Alisema kitakachofanyika ni kuimarisha usalama wa raia kupitia kamati yake ya ulinzi na usalama ya mkoa. 

Pia, alisema atatangaza kupiga marufuku uvutaji sigara hadharani zaidi kwenye mikusanyiko na kupambana na vijana na watu wanaojihusisha na uvutaji wa shisha (bangi).

“Mtu asiyevuta sigara, anakerwa sana na moshi ndiye anayeathirika zaidi, nitatangaza rasmi hivi karibuni marufuku ya kuvuta sigara, sasa watu watafute kwa kuvutia… nitatangaza na hatua za kuchukua,” alisema. 

Makonda alitumia nafasi hiyo kuwataka NMB kuchangia madawati, kwa shule za msingi na sekondari katika mkoa wake.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa NMB, Ineke Bussemaker alisema utamaduni wa kufuturu pamoja hasa katika Afrika unadumisha amani, umoja na upendo miongoni mwa Waislamu na watu wengine, hivyo wao wanauendeleza.
Hatima ya shauri lililofunguliwa na Chadema dhidi ya Polisi kupinga amri ya kupiga marufuku maandamano na mikutano ya kisiasa itajulikana Juni 21, Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza itakapotoa uamuzi kuhusu pingamizi lililowasilishwa na upande wa utetezi kuomba litupiliwe mbali.

Jaji Mohamed Gwae anayesikiliza shauri hilo, alifikia uamuzi huo baada ya kusikiliza hoja za mawakili wa pande zote za utetezi na mleta maombi.

Awali, Mawakili wa utetezi, Robert Kidando na Obadia Kajungu waliomba Mahakama kutupilia mbali maombi ya Chadema kuruhusiwa kufungua kesi yaliyowasilishwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, kwa madai kuwa hayajakidhi mahitaji ya kisheria.

Akifafanua, Wakili Kidando alidai mleta maombi hajataja baadhi ya vifungu muhimu ikiwamo kifungu cha 5(1)(2), vinavyoipa Mahakama mamlaka ya kisheria kusikiliza na kuamua maombi hayo.

Madai hayo yalipingwa na mawakili wa Chadema; Gasper Mwanaliela na John Mallya waliodai hoja za wajibu maombi hazina uhalali kisheria kwa sababu hati ya maombi yaliyopo mbele ya Mahakama yamekidhi mahitaji ya kisheria.

Wakili Mallya alidai kisheria, hati ya maombi inapaswa kuwa na vitu vitatu muhimu; hati ya kiapo, maelezo ya mleta maombi na ombi la shauri kusikilizwa kama inavyoelekezwa na kifungu cha 5(3).

Wakili Mallya aliomba Mahakama kutupilia mbali pingamizi la upande wa utetezi na kumpa nafuu mleta maombi, kesi yake kusikilizwa na kuamuliwa.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Jaji Gwae aliahirisha shauri hilo hadi Juni 21, Mahakama itakapotoa uamuzi huku akiuagiza upande wa utetezi kuwasilisha hati kinzani kujibu hoja za mleta maombi.

Katika maombi ya msingi, Chadema inaomba Mahakama kutamka kuwa amri ya polisi na utekelezaji wake ni batili, kwa sababu ni kinyume cha katiba na sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 1992.
TANZANA kwa sasa inajikita zaidi katika utafiti wa madini yanayohitajika zaidi duniani yakiwemo yanayotumika kutengeneza vifaa vya simu na betri za magari, Bunge linaloendelea na vikao vyake mjini Dodoma limeambiwa.

Aidha katika juhudi hizo, madini aina ya helium (he) yanayotumika kwa ajili ya mitambo ya Apollo na pia kutumika kwenye vifaa vya matibabu kama MRI na NMR yamegundulika kuwepo nchini Tanzania.

Akijibu maswali ya wabunge jana, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, alisema kwamba baadhi ya madini kama chuma na shaba, uhitajikaji wake duniani umepungua sana kwa sasa.

Katika maswali yao, Mbunge wa Igunga (CCM), Dalaly Kafumu alitaka kuthibitishiwa kuhusu uwepo wa taarifa kwamba utafiti wa madini nchini mwetu umepungua sana.

Akijibu swali hilo, Profesa Muhongo alitoa ufafanuzi kwamba madini yamekuwa yakitafutwa kwa vipindi na yanapokuwa mengi, uhitajikaji wake hupungua sambamba na utafiti.

Alifafanua kwamba katika miaka hii uhitaji wa baadhi ya madini kama shaba na chuma umepungua sana.

“Ndio maana utaona hata uchumi wa Zambia umeyumba kwa sababu China ambayo ndio mnunuzi mkubwa wa shaba kutoka nchini humo imepunguza mahitaji ya madini hayo,” alisema Muhongo.

Alisema madini yanayotengeza vifaa vya simu (rare earth mineral) na yale yanayotengeza betri (graphite) yataendelea kutafutwa kila mara kutokana na uhitajikaji wake na ndio maana akasema Tanzania nayo inajikita zaidi katika kusaka madini hayo.

Alifafanua kwamba madini hayo yanayotengeneza betri za magari yataendelea kuhitajika sana kwa sababu ulimwengu wa sasa unajikita zaidi katika kutengeneza magari yanayotumia umeme kwa wingi.

Kuhusu madini ya helium ambayo huwa katika mfumo wa gesi inayopatikana katika kina kifupi, Waziri Muhongo alifafanua kwamba utafiti ulifanywa na vyuo vikuu vya Oxford na Durham ulithibitisha kwamba kuna madini hayo nchini.

Alifafanua kwamba kiwango kilichogunduliwa cha madini hayo katika Ziwa Rukwa ni mita za ujazo bilioni 52.2 na kwamba utafiti zaidi unaendelea. Kwa sasa nchi inayozalisha kwa wingi madini hayo ni Marekani ambako hata hivyo, Profesa Muhongo, alisema yamekuwa yakipungua siku hata siku.