Saturday, 6 August 2016


Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA Mhe. Tundu Lissu alipewa dhamana saa tatu usiku wa kuamkia leo  katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, baada ya kukana mashitaka matatu ya uchochezi aliyosomewa.

Lissu alitimiza masharti ya dhamana baada ya mvutano mkali wa zaidi ya saa 5 na kujidhamini mwenyewe kwa dhamana ya shilingi milioni 10, na kesi yake imeahirishwa hadi Agost 19, 2016.

Mapema jana Katika Mahakama ya Hakimu MkazI Kisutu, ulinzi uliimalishwa tangu saa mbili asubuhi ambapo askari polisi waliokuwa na silaha walikuwa wakizunguka huku na huko kuhakikisha wafuasi wa chama hicho hawakusanyiki katika eneo la mahakama, huku kukiwa na matarajio ya kuwa wakati wowote atafikishwa mahakamani hapo.

Viongozi mbalimbali wa chama hicho nao walikuwepo katika mahakama hiyo kufuatilia kesi hiyo ya Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki.

Majira ya saa nane mchana Mhe Lissu alifikishwa mahakamani na kupandishwa kizimbani.

Akisomewa Mashataka na Wakili wa Serikali Paul Kaduche mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Cyprian Mkahe ilielezwa kuwa Mhe Tundu Lissu alifanya makosa hayo matatu Agost 2 mwaka huu, katika maeneo ya mahakama hiyo, kwa kutoa maneno ya uchochezi, maeneno ya dharau katika mfumo wa utoaji haki pamoja na kuidharau mahakama ya Kisutu.

Mshtakiwa alikana mashtaka hayo na baadaye ukatokea mvutano mkali wa kisheria juu ya uhalali wa dhamana ambapo mawakili wa serikali walikuwa wakipinga mtuhumiwa huyo kupewa dhamana.

Baada ya mvutano wa zaidi ya saa 5, kuanzia saa 10 jioni hadi saa tatu usiku,  hakimu alikubali hoja za upande wa utetezi na kutoa dhamana baada ya Lissu kukamilisha masharti ya dhamana hiyo.

Mara baada ya kuchiwa, Lissu akiongozana na baadhi ya viongozi wa chama chake, aliondoka mara moja mahakamani hapo.

Advertisement
==

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Mpekuzi Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka

Oparesheni UKUTA Ya Chadema Yapigwa Marufuku Dar es Salaam

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda ameliagiza jeshi la polisi mkoa wa Dar es salaam kuhakikisha kwamba sheria zinafuatwa na kusiwepo kitu kinaitwa UKUTA ili wananchi waendelee na kazi zao kama kawaida.

Akizungumza jana na kikosi cha kutuliza ghasia katika kambi ya Ukonga Jijini Dar es salaam Mkuu wa Mkoa alisema kwa kuwa askari wanafahamu sheria wasisubiri mtu yeyote kuja kuwakumbusha juu ya jambo hilo au maelekezo mengine kwa kuwa Amiri Jeshi ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameshaagiza kinachotakiwa ni utekelezaji.

‘’Msisubiri maelekezo yoyote kutoka juu, asiwepo mtu yeyote akafunga duka kwa sababu ya UKUTA, nyie ni matrekta hakuna UKUTA unaweza kusimama mbele yenu, mimi kama Mkuu wa Mkoa ninaamini hatutakuwa na vurugu kwenye Mkoa wetu na hatuwezi kuruhusu vurugu kwa kuwa tunajua madhara ya vurugu’’ Alisema Makonda.

Aidha kwa upande wake Kamanda wa Oparesheni Kanda Maalum ya Dar es Salaam Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Lucas Mkondya alisema jeshi la polisi lipo vizuri na vijana wameandaliwa vizuri na wameandaliwa kuwa tayari siku nyingi na hakuna mtu yeyote atakayethubutu kufanya UKUTA na watakaofanya hivyo watazimwa kabla hawajafanya chochote.

Kamada aliwataka wananchi wote Jijini Dar es Salaam kuto jitokeza kwenye oparesheni UKUTA kwa kuwa maandamano hayo siyo halali na watakaojitokeza watapata matatizo yasiyowahusu.

Oparesheni UKUTA ilitangazwa na CHADEMA ikiwa na maana Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania na ikatajwa tarehe Mosi Septemba nchi nzima chama hicho kitafanya mikutano ya hadhara jambo ambalo limepingwa na serikali kuanzia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kufuatia wakuu wa mikoa.