Thursday, 31 March 2016



Mwenyekiti wa Kitongoji cha Bweya katika Kijiji cha Bweya mkoani Geita, Augustine Katemi (42) ameuawa baada ya kufumaniwa akifanya mapenzi na mke wa mtu vichakani.

Mwenyekiti huyo alifariki dunia papohapo baada ya kudaiwa kushambuliwa kwa sime na mume wa mwanamke huyo, mkazi wa Kijiji cha Luchili, Wilaya ya Buchosa mkoani Mwanza.

Tukio hilo lilitokea saa nne usiku Machi 28 baada ya marehemu kudaiwa kukutwa akifanya tendo la ndoa na Chausiku Isangula (32).

Hata hivyo, alipoulizwa kuhusu tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Latson Mpojoli alisema  hana za taarifa za tukio hilo na kuahidi kufuatilia.

Ilielezwa kuwa Katemi aliuawa baada ya kushambuliwa kwa sime na kufa papohapo na baada ya tukio hilo, mtuhumiwa anadaiwa kumshambulia mkewe kwa kutumia sime hiyohiyo na kumsababishia majeraha makubwa sehemu mbalimbali za mwili na amelazwa kwenye Kituo cha Afya cha Nzera.

Mtendaji wa Serikali ya Kijiji cha Bweya, Samson Walwa alisema baada ya kutokea tukio hilo wananchi waliendesha msako na kumtia mbaroni mtuhumiwa wakati akijaribu kutoroka kuelekea Sengerema.

Walwa alisema mtuhumiwa alikamatwa nyumbani kwa Edward Iswalala alipokuwa amefikia kwa siri kutoka Luchili ili kufuatilia mwenendo wa mkewe ambaye anadaiwa kuwa awali alimuaga kuwa anakwenda kumsalimia baba yake mzazi anayetibiwa kwa mganga wa kienyeji.

“Inavyosemekana alikuwa akifuatilia mienendo ya mke wake… sisi tulipomkamata tumemkabidhi Kituo cha Polisi cha Nzera pamoja na nguo za marehemu (mwenyekiti) na zile za mkewe kwani alipofanya mauaji hayo alizichukua nguzo zao hadi tulipomkata nazo,” alisema Walwa.

Mmoja wa wananchi walioshuhudia tukio hilo, Jumanne Tole alisema, Chausiku alimuaga mumewe kuwa alikuwa anakwenda kijiji cha Kalebezo kumsalimia baba yake mzazi kwa waganga wa tiba asilia alikokuwa anatibiwa lakini baada ya kufika na kumsalimia, alikwenda kwa kaka yake aitwaye Ndagabwene Isangula huko Bweya alikofikwa na mkasa huo.

Alisema kuna madai kuwa mtuhumiwa alifika kijijini hapo kwa siri akiwa amevaa nguo na kofia zilizochakaa ili asifahamike wakati akifuatilia nyendo za marehemu na mkewe na akafanikiwa ikidaiwa kwamba alikuwa na watu ambao walikuwa wakimpatia taarifa hizo.
==

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Mpekuzi Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )


Kondakta wa daladala, Hamim Seif (42) mkazi wa Mwananyamala Ujiji, amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na shtaka la kutishia kumuua Rais John Magufuli kwa maneno.

Seif alipandishwa kizimbani mahakamani hapo jana mchana na kusomewa shtaka hilo na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Kenneth Sekwao.

Mshtakiwa huyo alikana shtaka hilo na Hakimu Mkazi, Hellen Liwa alisema kuwa dhamana ya mshtakiwa huyo iko wazi na alitakiwa kuwa na wadhamini wawili, kutoka taasisi ya Serikali inayotambulika, ambaye atasaini hati ya dhamana ya Sh2 milioni.

Licha ya dhamana yake hiyo kuwa wazi, mshtakiwa huyo alishindwa kukamilisha masharti hayo kwani baada ya kusomewa mashtaka alipoulizwa kama alikuwa na wadhamini alishindwa kuwapata.

Akimsomea shtaka linalomkabili, Wakili Sekwao alisema kuwa mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo Machi 10 mwaka huu katika baa ya Soweto, Makumbusho wilayani Kinondoni kinyume cha kifungu cha 89 (2) (a) na kifungu cha 35 cha Sheria ya Kanuni za Adhabu.

Wakili Sekwao alisema akiwa katika baa hiyo, mshtakiwa alitishia kumuua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Magufuli kwa maneno kwa njia ya kujitoa mhanga.

Kwa haya mambo anayoyafanya Rais Magufuli, mimi nimo tayari kujilipua kwa kujitoa mhanga ili kumuangamiza,” alisema Wakili Sekwao akimnukuu mshtakiwa huyo.

Hata hivyo, Wakili Sekwao alisema upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na akaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kesi hiyo kutajwa.
==

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Mpekuzi Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka

Balozi wa China nchini Tanzania Dkt. LU Youqing amefanya mazungumzo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano na Mazingira Mh. January Makamba Ofisini kwa Waziri huyo Mtaa wa Luthuli jijini Dar es Salaam.

Katika mazungumzo yao Balozi wa China amesema kuwa Serikali ya China inaamini kwamba uchaguzi wa Zanzibar uliofanyika mwishoni wa wiki iliyopita ulikuwa huru na haki. 
Balozi Youqing amesema kuwa Makamu wa Rais wa China ametuma salamu za pongezi kwa Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein kwa kuchaguliwa kwake na kwa watu wa Zanzibar kwa kuendesha uchaguzi huo katika misingi ya haki na uhuru. 
“Alikuwepo shuhuda wetu katika kushuhudia uchaguzi huo na alituambia kuwa ulikuwa wa haki na uhuru,” alisema Balozi huyo.

Katika mazungumzo hayo Balozi Youqing alisema Serikali ya China itaendelea kutoa misaada na kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwani huo ni wajibu wa mataifa makubwa kwa nchi zinazoendelea. 
Alimhakikishia Mheshimiwa Makamba kwamba China ina mipango mingi ya ushirikiano na Tanzania, ikiwemo kwenye sekta ya umeme na itaendelea kutoa ushirikiano kwa Tanzania, ikiwemo kupitia makampuni ya China, ili kuhakikisha malengo ya Tanzania kwenye sekta ya umeme yanatimia.

Kwa upande wake, Mheshimiwa Makamba alimshukuru Balozi Youqing pamoja na Serikali ya China kwa ushirikiano uliopo baina ya nchi hizo mbili.
 “Ujumbe na salamu ulizotoa leo umetupa faraja Watanzania. Urafiki baina ya nchi zetu, na baina ya vyama vyetu vya CCM na CCP, ni wa muda mrefu, ni wa majira yote, na umejengwa kwenye misingi ya kuheshimiana na hauna budi kuendelezwa”, alisema Mheshimiwa Makamba.

Pia Waziri Makamba na Balozi Youqing walikubaliana kutembelea Pemba na Unguja kwa pamoja mwezi Aprili ili kukagua na kutengeneza miradi ya maendeleo kati ya China na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Vilevile, walikubaliana kuhusu kutengeneza mradi mkubwa wa ushirikiano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muugano wa Tanzania na China kwenye teknolojia zitakazosaidia kupunguza matumizi ya mkaa, hivyo kuhifadhi mazingira.

Waziri Makamba pia amemueleza Balozi Youqing kuhusu hitaji na umuhimu wa ushirikiano katika kuiwezesha Tanzania kumiliki teknolojia ya uzalishaji wa nishati kwa kutumia taka ngumu zinazozagaa katika miji ya Tanzania ambapo Balozi Youqing aliahidi kulifuatilia suala hilo.

IMETOLEWA NA:
KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI,
OFISI YA MAKAMU WA RAIS.

==

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Mpekuzi Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka


James Lembeli (Chadema ) Aangukia Pua Kesi ya Kupinga Ushindi wa Mbunge wa CCM Kahama


Mahakama kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga leo imetupilia mbali maombi ya James Lembeli wa CHADEMA ya kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi wa mbunge wa Jimbo la Kahama Mjini wa Oktoba 25 2015, kwa madai kwamba taratibu zilikiukwa.

Akisoma hukumu iliyochukua saa tatu Jaji wa Mahakama hiyo Moses Mzuna amesema ushahidi uliotolewa na upande wa Lembeli haukuwa na nguvu za kutosha kuishawishi mahakama hiyo kutengua matokeo ya uchaguzi kwani sehemu kubwa ni wa maneno.

Jaji Mzuna amesema kitendo cha Lembeli kulalamikia vitendo vya rushwa vidavyodaiwa kufanywa na mgombe wa kiti hicho kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jumanne Kishimba kushindwa kuvitolea taarifa kwenye vyombo vya dola kimedhoofisha ushahidi na kuuwekea mashaka. 
Kwa upande wa mashahidi waliounga mkono kuwepo kwa vitendo vya rushwa Jaji Mzuna amesema wameshindwa kujenga hoja kwa mlolongo unaofanana kiasi kwamba wameonekana kana kwamba walikuwa na ushahidi wa kutengenezwa.

Akitoa hukumu hiyo, Jaji Mzuba amefafanua kuwa madai ya unyanyasaji wa wafuasi wake waliokamatwa na polisi katika hoteli ya Golden Rock na wengine katika kata ya Ngogwa yamekosa nguvu kufuatia kukosekana kwa kielelezo cha maandishi kinachoonesha kwamba walikuwa mawakala wake.

Mzuna amesisitiza, sababu ya Lembeli kushindwa kupeleka malalamiko kwenye kamati ya maadili ya uchaguzi iliyowekwa kisheria kwamba hakuwa na muda wa kutosha haikubaliki kwa kuwa mpiga kura yeyote anayemuunga mkono angeweza kulalamika.

Kufuatia uamuzi huo wa mahakama kutupilia mbali maombi ya kutengua matokeo hayo Lembeli amesema anaiheshimu mahakama, na kwamba atashauriana na wakili wake kuona kama haki haikutendeka ili kukata rufaa.

Naye Mbunge wa Jimbo la Kahama Mjini aliyekuwa mlalamikiwa namba moja katika shauri hilo Kishimba alipohojiwa amesema Jaji ametenda haki kama walivyotenda haki wananchi wa Kahama kwa kumpa kura za ushindi katika uchaguzi wa oktoba 25,2015.

Shauri hilo lilikuwa limevuta hisia za wananchi wa Kahama na kuhudhuria kwa wingi leo kwenye hukumu yake huku makundi ya kisiasa yaani wana-CCM na wana-CHADEMA yakijionesha wazi kwa kushangilia bila dalili zozote za uvunjifu wa amani.
==

Bonyeza HAPA kudownload applicationi ya Mpekuzi Blog kwenye simu yako ili kupata habari zetu Haraka